Muongozo wa rasilimali Watu

Muongozo wa rasilimali watu ni majumuisho ya kanuni na taratibu za kiutendaji katika kampuni au ofisi zinazowekwa na mwajiri kwa ajili ya kutoa muongozo wa kiutendaji wa mfanyakazi katika mazingira ya kazi. Husaidia kuboresha amani na utulivu mahali pa kazi.

Ni upi muongozo wa rasilimali watu?

Muongozo wa rasilimali watu unaweza kua na majina mengi kama vile kitabu cha muongozo kwa mfanyakazi au muongozo kwa wafanyakazi. Muongozo huu ni majumuisho ya kanuni za kampuni zinazowekwa na mwajiri kwa ajili ya kuongoza utendaji wa mfanyakazi katika mazingira ya kazi. Husaidia kuboresha amani na utulivu mahali pa kazi.


Je ninabanwa na kanuni na sheria zilizowekwa na muongozo wa rasilimali watu?

Pale muongozo huu wa rasilimali watu unapokua rasmi; kwa maana kwamba umekubaliwa kwa sahihi ya pande  zote mbili yaani mwajiri na mfanyakazi basi unakua na nguvu ya kisheria. Muongozo huu unaongoza pande zote mbili za mwajiri na mfanyakazi. Inapotokea ukiukwaji wa muongozo huu upande utakaokua umefanya ukiukwaji huu utalazimika kupata adhabu inayohusiana na ukiukwaji huo. Inapotokea kuna utata katika kanuni hizo basi itadadafuliwa dhidi ya upande uliotengeneza kanuni hizi ambao ni mwajiri.

Je muongozo huu wa rasilimali watu unaweza kua na nguvu kuliko masharti na vigezo vilivyowekwa na sheria?

Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi, 2004 imeweka viwango vya chini vya ajira. Hii inamaanisha kwamba nyaraka za ndani kama muongozo wa rasilimali watu au mkataba wa ajira hauwezi kutoa kiwango cha chini zaidi ya kilichowekwa na sheria lakini zinaweza kuboresha au kutoa sawa na sheria ilivyosema. Muongozo wa rasilimali watu hautakiwi kukinzana na sheria ila unaruhusiwa kutoa vigezo vizuri zaidi ya vile vilivyoko kwenye sheria, kwa mfano: sheria imetoa siku 28 za likizo ya mwaka yenye malipo kila mwaka, hivyo muongozo wa rasilimali watu hauwezi kutoa siku  20 za likizo ya mwaka lakini unaweza kuboresha na kutoa siku zaidi ya 28 au kutoa siku 28 hizo hizo kama zilivyotolewa na sheria.

Je ni haki yangu mimi kama mwakilishi wa chama cha wafanyakazi au mwakilishi wa wafanyakazi kuhusishwa katika zoezi la kuandaa muongozo wa rasilimali watu?

Kutokana na kwamba muongozo wa rasilimali watu ni nyaraka za ndani za kampuni basi ni maamuzi ya mwajiri kuamua nani ahusishwe katika uandaaji wa nyaraka hii. Hata hivyo, muongozo huu ni lazima utayarishwe na watu wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya ajira na rasilimali watu. Kama mwajiri ataamua kuhusisha chama cha wafanyakazi au mwakilishi wa wafanyakazi kama hakuna chama anaweza kuamua ni katika hatua ipi awahusishe watu hawa kama ni toka mwanzo wa maanadalizi aua katika hatua ya mwisho ya kurejea kabla muongozo huo haujawa rasmi ili aweze kupata maoni yao. Hata hivyo kwa urahisi wa utekelezaji wa muongozo huu wa rasilimali watu inashauriwa kuwahusisha chama cha wafanyakazi au wawakilishi wa wafanyakazi katika hatua ya mwisho ya kurejea nyaraka hii kabla haijawa rasmi, hii itasaidia kupata maoni yao na kiapo chao cha kuiheshimu nyaraka hiyo.

Je mwajiri wangu anaweza kubadilisha muongozo wa rasilimali watu baada ya kua umetiwa sahihi na pande zote mbili?

Ndio, vipengele vya muongozo huu vinaweza kubadilishwa lakini kutokana na sababu kwamba muongozo huu ni wa pande zote mbili basi mpango wowote wa kubadili chochote katika nyaraka hii unatakiwa kuhusisha pande zote mbili. Hii inamaanisha kwamba mfanyakazi ni lazima ahusishwe katika ubadilishaji ili kuweza kutoa maoni yake na ruhusa ya mabadiliko. Kama mabadiliko haya yatafanyika bila kuhusisha wafanyakazi au chama chao hiyo itakua ni ukiukwaji wa vigezo vya muongozo huo uliofanywa na upande mmoja na mwajiri atawajibika na ukiukwaji huo.

Ni kwanini kunakua na muongozo wa rasilimali watu katika eneo langu la kazi?

Sheria inamtaka mwajiri kuonyesha haki za mfanyakazi katika sehemu iliyoko wazi au yenye urahisi wa kuiona katika mahali pa kazi. Kwa kuzingatia haya basi muongozo huu ni muhimu sana. Vile vile inashauriwa kua na huu muongozo kwani unapunguza uvunjifu wa amani na utulivu katika mahali pa kazi kwa kuonyesha masharti yote na adhabu itolewayo panapotokea ukiukwaji wa aina yoyote. Pia sheria haijitoshelezi katika kila suala linalohusu kazi kwa kiasi Fulani ipo kimya kwenye masuala kadha wa kadha. Muongozo huu wa rasilimali watu unaweza kusaidia kutoa ufafanuzi wa vipengele muhimu vilivyoacha na sheria, kwa mfano;  masuala ya huduma za matibabu, fedha za kujikimu unapokua nje ya eneo la kazi kikazi, masuala ya kunyonyesha n.k.

Soma zaidi:

Jaza tafiti ya mishahara usaidie upatikanji wa taarifa za mishahara katika fani tofauti

Fahamu kuhusu kima cha chini cha mishahara Tanzania

loading...
Loading...