Ubaguzi sehemu za Kazi

Fahamu yote kuhusu ubaguzi katika sehemu za kazi, ubaguzi na sheria za kazi, ubaguzi na sheria na mengine mengi juu ya kazi katika Mywage Tanzania.

Ni nini ubaguzi chini ya sheria za kazi za Tanzania?
Ubaguzi haujaelezewa kwa kina chini ya sheria za kazi za Tanzania lakini Kifungu namba 1 (a) na (b) cha Azimio Na. 111 juu ya Ubaguzi ( Ajira na Kazi) ya mwaka 1958 imeelezea ubaguzi ni pamoja na:


•    Utofauti, utenganishi au upendeleo wowote unaofanywa katika misingi ya uasili, rangi, jinsia, dini, mtizamo wa kisiasa, uasili wa kitaifa au jamii, ambao una madhara ya kuzuia au kunyima usawa katika fursa au utendewaji katika kazi au ajira.

•    Utofauti, utenganishi au upendeleo mwingine wowote wenye madhara ya kunyima au kuzuia usawa wa fursa au utendewaji katika ajira au kazi kama utakavyoamuliwa na muhusika baada ya ushauri na wawakilishi wa vyama vya Wafanyakazi au Waajiri pale ambapo vipo au kupitia vyombo vingine husika.

•    Kwa kuongezea, kifungu cha 7 (5) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004, inaeleza kwamba unyanyapaaji wa mfanyakazi unaweza kua aina ya ubaguzi na utazuiwa katika misingi ile ile kama ubaguzi dhidi ya rangi, utaifa, ukabila au eneo ulilotokea, uasili, uasili wa taifa, jamii uliyotokea, mtizamo wa kisiasa au dini, jinsia, hali ya ujauzito, hali ya ndoa au majukumu ya kifamilia, ulemavu, Virusi vya VVU na UKIMWI, umri na maisha anayoishi.

Je Sheria inazuia ubaguzi?
Kifungu cha 7 (4) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004, imekataza ubaguzi dhidi ya mfanyakazi katika sera yoyote ya ajira au utendaji katika misingi ifuatayo:


•    Rangi
•    Utaifa.
•    Kabila au mahali alipotokea.
•    Uasili.
•    Uasili wa Taifa.
•    Asili wa kijamii.
•    Mtizamo wa kisiasa au dini.
•    Mwanaume au mwanamke.
•    Jinsia.
•    Ujauzito.
•    Kuolewa au kutokuolewa au majukumu ya kifamilia.
•    Ulemavu .
•    VVU/UKIMWI.
•    Umri.
•    Maisha anayoishi.

Je kuna hali yoyote inayoweza kuonekana kama ubaguzi lakini sheria inaikubali?
Ndio. Hali zifuatazo zinaweza kuonekana kama ubaguzi lakini chini ya sheria zimeelezewa kama si ubaguzi:


•    kuchukua hatua za kiupendeleo ili kuleta usawa au kutokomeza ubaguzi katika   sehemu ya kazi
•    Kutofautisha, kuzuia au kupendelea mtu yeyote kwa msingi wa mahitaji ya asili ya kazi
•    Kuwaajiri raia kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Kukuza Ajira ya Taifa ya mwaka 1999.

Nifanye nini kama nimebaguliwa kusikokua na haki?
Kama unahisi umebaguliwa kusikokua kwa haki au mwajiri amekiuka sheria, unaweza kufungua malalamiko kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ndani ya siku 60 toka ubaguzi huo utokee. Kama tume haitakua na uwezo wa kusuluhisha kupitia usuluhishi, suala linaweza kupelekwa kwa ajili ya maamuzi au mahakama ya kazi kwa kutoa hukumu. Kama ubaguzi huo utakua umefanywa na mfanyakazi mwenzake basi suala hilo litashughulikiwa ndani kwanza kama malalamiko.

Ni jukumu gani sheria imemwekea mwajiri kuhakikisha kwamba hakuna ubaguzi katika sehemu za kazi?
Sheria inamuhitaji mwajiri kusimamia fursa sawa katika ajira na kuhakikisha anaondoa ubaguzi katika sera za ajira na utendaji. Mwajiri anahitajika kutoa mpango wa kusimamia fursa sawa na kuondoa ubaguzi kwa kamishna wa kazi.


Ni nani mwenye majukumu ya kutoa vithibitisho katika kesi ya ubaguzi niliyofungua dhidi ya mwajiri wangu?
Pale mfanyakazi anapofungua kesi ya ubaguzi dhidi ya mwajiri katika misingi yoyote kama ilivyoelezwa hapo juu, itakua ni jukumu la mwajiri kutoa ushahidi kwamba ubaguzi haukufanyika au kitendo hicho hakiendani nay ale yaliyotajwa hapo juu.


Je ubaguzi unakatazwa katika ajira pekee?
Hapana! Ubaguzi umekatazwa dhidi ya mwombaji wa kazi katika kipindi cha kuchaguliwa na kuitwa kwenye usahili pamoja na yule aliyeajiriwa. Kamati ya kuchagua na kufanya usahili inatakiwa kujitahidi kuhakikisha kwamba uchaguzi wao haujafanywa kutokana nay ale yaliyotajwa hapo juu.

Soma zaidi

Fahamu zaidi juu ya kima cha chini cha mishahara na ujaze tafiti ya mishahara

loading...
Loading...