Likizo ya Uzazi/Ulezi

fahamu kuhusu likizo ya uzazi/ulezi kutokana na sheria za kazi za Tanzania, malipo ya likizo za uzazi, stahili na mafao ya likizo ya uzazi, huduma za afya ya uzazi, haki ya mfanyakazi kuchukua likizo ya uzazi/ulezi, idadi ya likizo za uzazi/ulezi, fahamu yote kupitia Mywage Tanzania

Mbali na likizo ya mwaka, ni aina gani nyingine ya likizo ninastahili?
Mbali na likizo ya mwaka mfanyakazi pia anastahili likizo ya uzazi (kwa Mama) au ulezi (kwa baba), likizo ya ugonjwa na likizo ya kuuguliwa ama kufiwa. Hizi ndo aina za likizo zilizoainishwa na sheria. Hata hivyo majadiliano ya pamoja au sera za ndani ya ofisi zinaweza kuainisha aina zaidi za likizo. 


Ni kwa vipi ninastahili likizo ya uzazi/ulezi? 
Likizo ya uzazi inaelezewa chini ya Sehemu ndogo D ya Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004. Mfanyakazi atastahili likizo ya uzazi/ulezi baada ya kumaliza miezi sita (6) kazini toka siku mkataba wa kazi ulipoanza. Kigezo kingine cha mfanyakazi kustahili likizo ya uzazi/ulezi ni masharti ya sheria yanayomuhitaji mfanyakazi kutoa taarifa ya maandishi kwa mwajiri juu ya dhamira yake ya kuchukua likizo ya uzazi angalau miezi mitatu (3) kabla ya siku anayotarajia kujifungua. Taarifa hiyo ni lazima iambatane na cheti cha madaktari.
Mfanyakazi atastahili likizo ya uzazi/ulezi baada ya kumaliza miezi sita (6) kazini toka siku mkataba wa kazi ulipoanza. 


Je mwajiri anaweza kuninyima likizo ya uzazi /ulezi kwa kushindwa kutoa taarifa kama inavyotakikana?

Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 imeweka kigezo hiki kwa mfanyakazi kuweza kupata likizo ya uzazi/ulezi. Sheria iko kimya juu ya kitakachotokea kama utashindwa kutoa taarifa kama inavyotakikana. Kwa hivyo inashauriwa kwa mfanyakazi kutoa taarifa ya miezi mitatu kwasababu mwajiri anaweza kukataa kutoa likizo ya uzazi/ulezi yenye malipo kwasababu ya kushindwa kufata taratibu zilizowekwa na sheria. 


Je, ninastahili siku ngapi za likizo ya uzazi/ulezi?

Katika mzunguko wa likizo ( kipindi cha miezi 36) unastahili siku 84 za likizo ya uzazi yenye malipo kama umepata mtoto mmoja au siku 100 za likizo ya uzazi yenye malipo kama umepata mtoto zaidi ya mmoja. Siku hizi zinajumuisha siku za mapumziko na sikukuu za kitaifa. Hata hivyo kama umepata matatizo yoyote kutokana na kujifungua na unahitaji siku za ziada unaweza kujadili na mwajiri kuona uwezekano wa kutumia likizo ya ugonjwa, ama siku kadhaa kutoka katika likizo yako ya mwaka au kupata siku zaidi bila ya malipo.
Kipindi cha likizo ya ulezi ( kwa baba) ni siku tatu katika mzunguko wa likizo ambao ni miezi thelathini na sita (36). Siku tatu hizi ndio jumla ya siku za mapumziko ya ulezi bila kujali idadi ya watoto waliozaliwa ndani ya mzunguko wa likizo. 


Je kuna hali yoyote chini ya sheria ambayo ikitokea itaniruhusu kupata siku 84 zaidi za likizo ya uzazi yenye malipo ndani ya mzunguko wa likizo?
Ndiyo, Kama utapata mtoto na mtoto akafariki ndani ya mwaka utastahili siku 84 zaidi za likizo ya uzazi yenye malipo. 


Je kuna kikomo cha idadi ya kuchukua likizo ya uzazi?
Kulingana na sheria zinazosimamia sekta binafsi mfanyakazi anaweza kuchukua likizo za uzazi/ulezi hadi mara nne katika kipindi chote cha ajira na mwajiri mmoja. 


Inapotokea nimemaliza likizo zangu za uzazi na nikabeba mimba tena, Je naweza kuomba likizo ya uzazi yenye malipo?
Huwezi kukataliwa likizo ya uzazi ila utapewa likizo ya bila malipo. 


Ni wakati gani naweza kuanza likizo ya uzazi/ulezi?
Mfanyakazi anaweza kuanza likizo yake ya uzazi wakati wowote kutoka wiki nne kabla ya siku anayotegemea kujifungua au mapema zaidi kama itathibitishwa na daktari kwamba ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto aliye tumboni.
Kwa upande wa likizo ya ulezi inatakiwa kuchukuliwa ndani ya siku saba (7) toka kuzaliwa kwa mtoto. 


Naweza kusitishwa/kuachishwa kazi wakati nikiwa mjamzito au mapema baada ya kurudi kazini kutoka likizo ya uzazi?
Ndiyo, unaweza kuachishwa kazi wakati ukiwa mjamzito ama mapema baada ya kurudi kazini kutoka likizo ya uzazi lakini sababu isiwe inahusiana na ujauzito wako au kujifungua. Mwajiri anaweza kukuachisha kazi kwasababu kama vile mwenendo mbaya au kufanya kazi katika kiwango cha chini lakini baada ya kufuata taratibu zilizowekwa na sheria.

Je kuna malipo yoyote ninayostahili chini ya sheria kutoka kwa mwajiri wangu wakati wa likizo ya uzazi?

Mwajiri anatakiwa na sheria kumpa mfanyakazi mwenye likizo ya uzazi mshahara wake wa kawaida ambao anastahili kama angekua kazini. Hata hivyo kama stahili za zaida zimetolewa chini ya sera za ndani za kampuni basi mwajiri atalazimika kulipa. 


Je mwajiri anawajibika na gharama zangu za hospitali zinazohusiana na ujauzito au kujifungua?

Sheria inaeleza kwamba mwajiri anawajibu wa kushughulikia gharama za matibabu za mfanyakazi kama mfanyakazi anaishi katika nyumba ya mwajiri au suala la gharama za matibabu limejadiliwa na kuwekwa katika makubaliano ya pamoja au kama mwajiri ana sera za ndani zinazoruhusu huduma za afya kwa mfanyakazi. 


Taasisi gani nyingine inaweza kugharamia stahili zangu za uzazi?
Mifuko kadha ya hifadhi ya jamii kama vile mfuko wa Taifa wa jamii (NSSF) una kipengele juu ya stahili za uzazi. Stahili za uzazi zina misingi miwili, Huduma za afya ya uzazi na Mafao ya Fedha Taslimu. Mwanamke ambaye ni mwanachama wa NSSF anaweza kupata haya kama amefikia viwango vifuatavyo:
•    Katika kipindi cha kujiandikisha uanachama na mfuko na wiki anayotarajia kujifungua ni lazima awe amelipa michango 36.
•    Kati ya michango 36 michango 12 lazima iwe imefanyika karibu na wiki ya kujifungua.
Kama masharti yote yatatimizwa basi mwanachama (mwanamke) atapata stahili zote. Kama sharti mojawapo halitatimizwa hatopata stahili hata moja. 

loading...
Loading...