Kazi na Uzazi - Kimataifa

Ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi katika kazi unawapa fursa wanawake kuchanganya kazi na majukumu yao ya kifamilia kama vile ujauzito n.k bila ya kuhatarisha moja kwa ajili ya nyingine. Vile vile inawalinda wanawake dhidi ya ubaguzi katika soko la ajira. Fahamu yote haya kupitia mywage.org.tz

Ni yepi maazimio ya ILO juu ya ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi?
Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilianza kushughulika na masuala ya ulinzi wa haki za uzazi au wajawazito toka lilipoanzishwa na maazimio ya kwanza juu ya ulinzi wa uzazi yalikubaliwa katika mwaka ambao ILO ilianzishwa ( 1919). Azimio la ulinzi wa haki za uzazi au wajawazito (Na.3) linaeleza pamoja na mambo mengine haki za msingi za wajawazito kama wiki 12 za likizo ya uzazi yenye malipo ( kiwango cha malipo katika kipindi cha likizo hii kitapangwa na taasisi za serikali katika nchi husika), mapumziko ya kunyonyesha na ulinzi wa kazi kipindi cha ujauzito. Hata hivyo azimio hili lililenga wanawake walioajiriwa katika sekta binafsi na za umma za viwanda na biashara.

Azimio la pili lilipitishwa miaka 33 baadae yaani mwaka 1952 (Na.103) ambalo lilitanua wigo na kujumuisha wanawake wanaofanya kazi katika sekta zisizokua za viwanda pamoja na kilimo na wafanyakazi wa ndani. Vile vile azimio hili liliongeza likizo ( angalau wiki 12) ambazo zitatolewa pia kwa magonjwa yatokanayo na mimba. Azimio la 183 lililokubaliwa mwaka 2000 ndio azimio la karibuni zaidi linalohusu suala la ulinzi wa uzazi au wajawazito. Azimio hili limetanua wigo wa ulinzi wa haki za wajawazito na uzazi kwa wafanyakazi wote na kutoa angalau wiki 14 za likizo ya uzazi yenye malipo.

Ni kwa nini ulinzi wa haki ya wajawazito/wazazi ni muhimu?
Ulinzi wa haki ya wajawazito na wazazi ni muhimu kwani inamuwezesha mwanamke kuchanganya majukumu ya uzalishaji kiuchumi na kujenga familia bila ya kuhatarisha moja kwa ajili ya nyingine. Vile vile humlinda mwanamke dhidi ya unyanyapaaji katika soko la ajira kutokana na majukumu yao ya kujenga familia.

Ulinzi wa haki ya wajawazito na wazazi inachangia katika afya ya uzazi na watoto na hivyo kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya millennia (MDGs) namba 4 na 5. Vile vile ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi unalinda na kuongeza ajira za wanawake na uwepo wao katika soko la ajira na kuhakikisha ulinzi wa kipato kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha taslimu na mafao ya matibabu katika kipindi cha ujauzito na hivyo kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya millennia namba 1 na 3.

Jedwali hapo chini linatoa taarifa husika ya malengo ya maendeleo ya millenia na makusudio - Yanayoendana na suala la ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi

Malengo ya maendeleo ya mileniaMakusudioViashiria
Lengo 1: Kuondoa umasikini na njaa Kusudio 1.B: Kufikia ajira za kudumu zenye kuzalisha na kazi za staha kwa wote, ikijumuisha wanawake na vijana

1.4 Ukuaji wa pato la taifa (GDP) kwa mtu alieajiriwa

1.5 Wastani wa ajira na idadi ya watu

1.6 Uwiano wa waajiriwa wanaoishi chini ya dola 1 ya kimarekani (1$) kwa siku

1.7 Uwiano wa akaunti binafsi na mchango wa wanafamilia wanaofanya kazi katika ajira

Lengo 3: Kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake Kusudio 3.A: Kukomesha utofauti wa kijinsia katika elimu za msingi na sekondari kufikia mwaka 2005 na katika ngazi nyingine za elimu kufikia mwaka 2015

3.1 Wastani wa wasichana kwa wanaume katika shule za msingi, sekondari na vyuo

3.2 Mgawo wa ujira kwa wanawake katika sekta isiyokua ya kilimo

3.3 Uwiano wa nafasi zilizoshikiliwa na wanawake katika bunge la Taifa

Lengo 4: Kupunguza vifo vya watoto Kusudio 4.A: Kupunguza kwa theluthi mbili vifo vya watoto chini ya miaka 5 kati ya mwaka 1990 na 2015

4.1 Idadi ya vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka 5

4.2 Vifo vya watoto wachanga

4.3 Uwiano wa watoto wenye umri wa mwaka 1 wenye kinga dhidi ya surua

Lengo 5: Kuboresha afya ya uzazi

Kusudio 5.A: Kupunguza kwa robo tatu kiwango cha vifo vya wajawazito kati ya 1990 na 2015

Kusudio 5.B: Kufikia upatikanaji wa jumla wa huduma za afya ya uzazi kufikia 2015

5.1 Idadi ya vifo vya wajawazito

5.2 Uwiano wa uzalishaji uliofanywa na watoa huduma wenye ujuzi

5.3 Idadi ya matumizi ya dawa za kuzuia mimba

5.4 Idadi ya mimba za ujanani

5.5 Upatikanaji wa huduma za kliniki

( angalau mara 1 hadi mara 4)

5.6 Kushindwa kufikia mahitaji ya kupanga familia

Ni vipi vipengele vya ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi?
Kuna vipengele kadha wa kadha vya ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi ambapo likizo ya uzazi ni mojawapo. Vipengele hivi ni pamoja na ulinzi wa afya ya mama mjamzito na mwenye kunyonyesha, likizo ya uzazi, likizo inayouhusiana na magonjwa yatokanayo na ujauzito, utoaji wa fedha taslimu na mafao ya matibabu, ulinzi wa ajira na ubaguzi, kutoa ruhusa kwa mama anaenyonyesha. Malengo tajwa haya yatafikiwa kama tu nchi itaamua kutengeneza sheria inayolinda haki za wazazi na wajawazito na kuzisimamia ili kuhakikisha zinafuatwa na makampuni.

Je Shirika la Kazi Duniani (ILO) linasemaje kuhusu afya na usalama kipindi cha ujauzito?

Azimio 183 la Shirika la Kazi Duniani (ILO) linatambua haki za wajawazito na wenye kunyonyesha na kuzilinda. Taasisi za kitaifa zinatakiwa kutambua aina za kazi ambazo zinaweza kua na madhara kwa afya ya mama au ya mtoto. Hatua mojawapo muhimu ya kulinda afya ya mfanyakazi mwenye ujauzito ni mpangilio wa saa za kazi. Kwa kawaida wajawazito hupata unafuu (na hivyo hulindwa) na kazi za usiku na zile za muda wa ziada. Awali maazimio ya ILO yalikataza kazi za usiku kwa wanawake. Hata hivyo kama kigezo cha usawa wanawake hawawezi kuzuiwa kufanya kazi za usiku. Hivyo hata wafanyakazi wajawazito hawakatazwi kufanya kazi za usiku ila wanaruhusiwa kuamua wenyewe. Maamuzi ya kukataa mfanyakazi mjamzito kufanya kazi za usiku au katika muda wa ziada yanaitajika yatolewe kutokana na ushauri wa daktari ukithibitisha kwamba kazi za usiku au katika muda wa ziada haziendani na mimba au kunyonyesha.

Kama kazi itakua na madhara kwa afya ya mfanyakazi mwenye ujauzito au mtoto basi mfanyakazi huyu atahitajika kupatiwa kazi mbadala ( kama kumuhamishia katika nafasi salama). Hii pia inaweza kua ni pamoja na kubadilisha hali yake ya kufanya kazi na muda wa kufanya kazi. Hatahivyo, kazi hiyo mbadala haitakiwi kumpelekea kupunguzwa mshahara au mafao. Uamuzi huu hufikiwa pale tu uchambuzi utakapoonyesha kwamba kazi ina madhara makubwa kwa afya ya mjamzito au mtoto.

Je ILO wanasemaje kuhusiana na mapumziko kwa ajili ya kunyonyesha?
Kutokana na azimio la 183 la ILO, mfanyakazi mwanamke ana haki ya mapumziko au punguzo la muda wa kufanya kazi kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto. Taasisi za kitaifa ndizo zinazopanga kipindi na idadi ya mapumziko haya. Azimio la kwanza la ILO juu ya haki za ulinzi wa wajawazito na wazazi (Na.3), hatahivyo ilitoa mapumziko ya dakika 30 katika kila siku ya kazi.

Kama ilivyoelezwa na tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO), kunyonyesha mtoto mpaka umri wa miezi 6 na kidogo kidogo mpaka umri wa miaka 2 au hata zaidi ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto. Mapumziko haya ya kunyonyesha ni tofauti na mapumziko ya chakula cha mchana na mapumziko ya kawaida. Vile vile kuna maelezo juu ya upatikanaji wa maeneo ambapo wafanyakazi wanawake wanaweza kunyonyesha watoto wao. Kwa kawaida ni jukumu la mwajiri kutoa sehemu kwa ajili ya shughuli hii. Hatahivyo maeneo haya huwepo panapokua na idadi fulani ya wafanyakazi wanawake katika kampuni kama vile wanawake 50 au 100.

Je ILO inasemaje kuhusiana na likizo ya uzazi?
Kama ilivyoelezwa hapo juu, maazimio ya awali yametoa angalau wiki 12 za likizo ya uzazi. Hatahivyo, azimio la 183 la ILO linahitajia likizo ya uzazi ya angalau wiki 14 katika hizo wiki 6 huchukuliwa pale mtoto anapozaliwa. Kutokana na takwimu za ILO, asilimia 51% ya nchi zinatoa likizo ya uzazi ya angalau wiki 14, asilimia 35% ya nchi zinatoa wiki 12 mpaka 13 za likizo ambazo ni pungufu ukilinganisha azimio la 183 lakini bado ni sawa na azimio la 3 na 103. Ni asilimia 14% tu zinatoa likizo ya uzazi ambayo ni pungufu ya wiki 12. Asilimia 82% ya nchi za mashariki ya kati zinatoa likizo ya uzazi ya chini ya wiki 12. Asilimia 93% ya nchi za ulaya mashariki na kati ( ambazo si wanachama wa umoja wa ulaya - EU) zinatoa angalau wiki 18 za likizo ya uzazi.
Mfanyakazi mwenye ujauzito ana uhuru wa kuchukua likizo yake kwa masharti kwamba atachukua likizo ya lazima ya wiki 6 kufuatia kujifungua. Dhumuni ni kumlinda mfanyakazi huyu na msukumo wa kutaka kurudi kazini ambao unaweza kua na madhara kwa mama na mtoto.
Azimio la Shirika la Kazi Duniani (ILO) linaelezea juu ya kurefusha likizo ya uzazi kama kutatokea hali zisizo za kawaida katika kipindi cha ujauzito ama baada ya kujifungua. Hii ni pamoja na kuchelewa siku zinazotarajiwa kujifungua, uzazi wa kabla ya wakati, uzazi wa mapacha na kuumwa kwa mama au mtoto n.k.  

Je ILO wanasemaje kuhusu mafao ya fedha taslimu kipindi cha likizo ya uzazi?
Azimio la 183 la ILO linataka mfanyakazi apewe mafao ya fedha taslimu kipindi cha likizo ya uzazi. Katika nchi zilizoendelea, Marekani ni nchi pekee isiyo toa mafao ya fedha taslimu kipindi cha likizo ya uzazi. Azimio pia linaeleza kwamba mafao hayo ni lazima yaweze kumwezesha mwanamke kupata maisha bora yeye na mtoto wake. Kama fao hili litategemea na kipato cha zamani ( kwa kawaida miezi 12 iliyopita) kiasi cha fao kinabidi kiwe angalau theluthi mbili ya kipato hicho. Fao hili ni lazima lidumu kwa kipindi chote cha likizo ya uzazi.
Azimio la ILO pia linahitaji masharti ya kupata mafao haya yawekwe katika hali ambayo itaruhusu idadi kubwa ya wafanyakazi wanawake wataweza kukidhi na kupata fao hili. Masharti ya kupata fao hili yanaweza kua ni pamoja na kiwango cha chini ambacho mfanyakazi huyu amefanya kazi na kampuni fulani ( kipindi cha miezi 6 au mwaka 1), mara ngapi mfanyakazi ataruhusiwa kupata fao hili, malipo ya kiwango cha chini cha michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii n.k.

Nani anaelipa mafao haya? Mwajiri au Serikali?

Maazimio yote ya awali yanaeleza kwamba si jukumu la mwajiri pekee kulipa fao hili bali hata mifuko ya hifadhi ya jamii au mifuko mingine ya umma. Hii ni kwa sababu kwa kumuitaji mwajiri kulipa mafao haya inaweza ikapelekea mtizamo hasi kwa wafanyakazi wanawake kwani Waajiri wataona gharama kubwa pale anapomwajiri mwanamke. Na hii itapelekea wanawake kubaguliwa katika nafasi za kazi. Maazimio ya ILO yanaeleza kwamba sio jukumu la mwajiri pekee kulipa mafao haya.

Kuna mifumo mitatu inayoweza kutumika katika kutoa mafao haya katika kipindi cha likizo ya uzazi, inaweza kua kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, rasilimali za mwajiri au mchanganyiko wa fedha za umma au za hifadhi ya jamii na rasilimali za mwajiri. Kutokana na takwimu za ILO, katika nchi 167 ambazo zilifanyiwa utafiti karibia nusu yao zinatoa mafao ya fedha taslimu kupitia mfumo wa mifuko ya hifadhi ya jamii wakati asilimia 26% inawaamuru Waajiri kutoa fao hili. Mgawanyo wa gharama kati ya mifuko ya hifadhi ya jamii na Waajiri inafanyika kwa asilimia 17%.

Je wafanyakazi wanalindwa dhidi ya kufukuzwa kazi katika kipindi cha likizo ya uzazi?
Maazimio namba 3 na 103 ya ILO ( juu ya haki za kulinda wajawazito na wazazi) zinasema kwamba mfanyakazi mwanamke ambae yuko katika likizo ya uzazi hawezi kufukuzwa kazi. Azimio 183 la ILO, hatahivyo limetanua ulinzi huu pia katika kipindi cha ujauzito, kipindi cha kunyonyesha ambapo mfanyakazi mwanamke atakua amerudi kazini kutoka likizo ya uzazi. Maazimio ya awali yanatoa ulinzi kwa wafanyakazi wanawake walioajiriwa pekee ( ulinzi dhidi ya kufutwa kazi) hatahivyo azimio la sasa linatoa ulinzi pia kwa wale wanaoutafuta kazi ( wanawake wajawazito na wanawake wanaolea watoto wadogo). Baada ya kumaliza likizo ya uzazi wafanyakazi pia wana haki ya kurudi katika nafasi zao za kazi za awali kabla ya kwenda likizo hiyo.

Soma zaidi:

Soma zaidi kuhusu likizo ya uzazi/ulezi-Tanzania

Jaza tafiti yetu ya mishahara na uweze kufananisha mshahara wako na watu wa aina yako

loading...
Loading...